Thursday, September 3, 2015

Jeshi la Magereza nchini kushirikiana na asasi za kiraia katika kupunguza msongamano magerezani

Washiriki wa Kongamano la Wasaidizi wa Kisheria Magerezani kutoka Magereza Mkoani tanga wakiendelea na majadiliano katika Kongamano hilo linalofanyika Mkoani Morogoro kwa siku tatu.

Na, Lucas Mboje, Morogoro

Jeshi la Magereza nchini limeahidi kuendelea kushirikiana na Asasi ya Envirocare katika kuimarisha Madawati ya Msaada wa Kisheria Magerezani ili kuleta tija katika utatuzi wa changamoto ya Msongamano wa Mahabusu inayolikabili Jeshi hilo.

Kauli hiyo imetolewa jana Mkoani Morogoro na Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, John Casmir Minja alipokuwa Mgeni rasmi wakati wa hafla ya ufunguzi wa Kongamano la Wasaidizi wa Kisheria Magerezani na Mahabusi za Watoto.

Jenerali Minja amesema kuwa Serikali imeendelea kuchukulia kwa uzito stahiki suala la Msongamano wa Mahabusu Magerezani ikiwemo kushirikiana na Wadau wa Haki Jinai katika kupunguza changamoto ya Msongamano wa Mahabusu Magerezani.

"Napenda kutoa rai kwa Asasi zingine zenye malengo yanayofanana na Asasi hii nazikaribisha kuja kufanya kazi na Jeshi la Magereza kwani mwelekeo wa Jeshi kwa sasa ni Urekebishaji wa Wafungwa(From Prisons to Corrections) ambapo Jeshi la Magereza watafanya kazi kwa karibu na Asasi za Kiraia na Jamii kwa ujumla". Alisema Jenerali Minja.

Awali akimkaribisha Mgeni rasmi Mkurugenzi Mtendaji wa Envirocare, Bi. Loyce Lema amesema kuwa imekuwa ni faraja kwao kupata ushirikiano kama huo kutoka Jeshi la Magereza kwani umewezesha kutekelezwa kwa mradi huo wa kutoa Msaada wa Kisheria kwa Mahabusu waliopo Magerezani kwa matokeo chanya kwa muda mufupi.

Bi. Lema alisema kuwa mradi huo umetekelezwa kwa miaka mitatu(2012 - 2015) na umetekelezwa kwenye Magereza 20 na Mahabusu 04 za Watoto katika Mikoa 05 ambayo ni Mkoa wa Kilimanjaro, Arusha, Tanga, Morogoro na Dar es Salaam.

Asasi ya Envirocare kwa kushirikiana na Jeshi la Magereza ilifanya utafiti wa awali wa kuangalia hali halisi ya Msongamano katika Magereza yaliyopo katika Mikoa mitano ya mradi. Matokeo ya jumla ya utafiti huo yalionesha kuwa kuna tatizo kubwa la Msongamano ambao unasababishwa na idadi kubwa ya Mahabusu katika Magereza ya Mikoa hiyo.